Jumapili 25 Oktoba 2026 - 10:25
Imam wa Ijumaa wa Najaf Ashraf/ Fungueni Njia ya Al-Shaib

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi, katika khutuba ya Swala ya Ijumaa, amekosoa sera za kuongeza shinikizo dhidi ya Iran na ukiukaji wa mamlaka ya Iraq unaofanywa na ndege za Israel. Aidha, ameitaka serikali kuweka wazi sababu za kufungwa njia ya Al-Shaib, huku akisisitiza umuhimu wa kufunguliwa tena njia hiyo au kutolewa njia mbadala inayofaa ili kuzuia madhara ya kiuchumi kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf, alizungumzia masuala mbalimbali ya ndani, ya kikanda na ya kimataifa katika khutuba ya Swala ya Ijumaa aliyotoa katika Husainiya Kuu ya Fatimiyya, Najaf Ashraf.

Kuwaunga mkono wanafunzi wa Azerbaijan na kuhimiza mshikamano

Mwanzoni mwa khutuba yake, alizishukuru wizara za Iraq na ofisi ya gavana wa Najaf Ashraf kwa kuwakaribisha wanafunzi kutoka Azerbaijan, akilitaja jambo hilo kuwa ni aina ya kuonesha mshikamano na mataifa ya Kiislamu.

Imam wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf pia alipendekeza kwamba mikusanyiko ya kuonesha mshikamano na wananchi wa Azerbaijan iandaliwe katika ngazi mbalimbali za elimu, ikiwemo shule za msingi, shule za sekondari na vyuo vikuu.

Kuhimiza kuenezwa tenzi za kidini shuleni

Katika sehemu iliyohusu masuala ya ndani, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi alisifu kuimarika kwa utamaduni wa kuimba tenzi za kidini katika shule za msingi. Pia aliishukuru na kuipongeza menejimenti ya shule hizo kwa kuchukua hatua hiyo yenye thamani.

Ndege za Israel kukiuka mamlaka ya Iraq

Katika kuendelea na hotuba yake, aligusia masuala ya kiusalama na, akirejelea taarifa rasmi, alibainisha kuwa ndege za Israel zinaingilia anga ya Iraq.

Alieleza kuwa kitendo hicho ni uvamizi dhidi ya mamlaka ya kitaifa, ukiukaji wa sheria za kimataifa, pamoja na dharau kwa heshima na hisia za wananchi wa Iraq. Hivyo, aliitaka serikali kuchukua msimamo thabiti na makini dhidi ya ukiukaji huo.

Kupinga kufungwa njia ya Al-Shaib na shinikizo dhidi ya Iran

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi, akizungumzia mikusanyiko ya wananchi katika mji wa Al-Amarah kupinga kufungwa njia ya Al-Shaib na madhara ya kiuchumi yaliyotokana na hatua hiyo alisema kuwa; serikali haijatoa sababu inayokubalika ya kufungwa njia hiyo.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imesababisha kuwepo mtazamo hasi na inaeleweka kana kwamba kuna nia ya kuongeza shinikizo dhidi ya Iran.

Akielezea mshikamano wake na wananchi wa Al-Amarah, alitaka mpaka huo ufunguliwe mara moja au njia mbadala inayofaa itolewe, huku akisisitiza pia umuhimu wa kuweka wazi kwa umma sababu za kuchukuliwa uamuzi huo.

Mfumo wa dunia unakaribia kuporomoka na Marekani kukabiliwa na kushindwa

Katika masuala ya kimataifa, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf, akigusia misukosuko ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi barani Ulaya, alisema kuwa hali hiyo ni ishara ya kukaribia kuporomoka kambi ya Magharibi.

Pia alisisitiza kuwa makabiliano ya Marekani dhidi ya Iran yamesababisha kile alichokiita “kushindwa Marekani kisiasa na kiuchumi”, huku akieleza kuwa Marekani ndiyo mhusika mkuu wa kupanda kwa bei duniani. Aliongeza kuwa dunia inakaribia kuporomoka kwa mfumo wa kimataifa unaotawaliwa na Marekani.

Trump kulidhalilisha jina la Mtume (s.a.w.w.): Ishara ya kuenea kwa Uislamu

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi pia aligusia matamshi ya Trump yenye kumkashifu Mtume wa Uislamu (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Ahlul-Bayt wake). Alieleza kuwa matamshi hayo ni ishara ya kuenea ushawishi wa Uislamu na hofu iliyopo kuhusu kukua mwamko wa Kiislamu katika kukabiliana na ubeberu wa kimataifa.

Khutuba ya kidini: Fadhila za Hadhrat Fatima Zahra (s.a.) katika vyanzo vya Ahlus-Sunna na Shia

Katika sehemu ya pili ya khutuba yake, iliyohusu masuala ya kidini, khatibu wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf, huku akigusia siku za kumbukumbu ya kuuawa kishahidi kwa Bibi Fatima Zahra (amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake), aliangazia nafasi na hadhi yake katika vyanzo vya Ahlus-Sunna na Shia.

Akitumia riwaya zinazotegemewa, alizungumzia hadithi isemayo: “Fatima ni sehemu ya mwili wangu”, iliyonukuliwa katika vitabu vya Sahih al-Bukhari na Sahih Muslim, pamoja na hadithi isemayo: “Fatima ni bibi wa wanawake wa watu wa Peponi”, iliyonukuliwa katika Sahih al-Bukhari.

Vilevile, aligusia kufanana kwa tabia na mwenendo wa Bibi Fatima Zahra na Mtume Mtukufu (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Ahlul-Bayt wake), huku akitegemea riwaya zilizopokewa na Tirmidhi na Abu Dawud.

Mwisho wa khutuba yake huku akitaja riwaya zilizopokewa katika vyanzo vya Shia, alisisitiza uhusiano wa kina uliokuwepo kati ya Mtume (s.a.w.w.) na Bibi Fatima Zahra (s.a.). Pia alisisitiza umuhimu wa uchamungu katika kufikia utulivu na baraka.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha